Picha kwa Hisani –
Baraza la Magavana nchini, sasa linatishia kuzifunga serikali za kaunti kutokana na bunge la seneti kushindwa kuutatua mvutano wa mfumo mpya wa ugavi wa raslimali kwa serikali hizo.
Baraza hilo linaloongozwa na Mwenyekiti wake Wycliffee Oparanya, limesema iwapo Kamati ya maseneta 12 waliotwikwa jukumu la kusawazisha mvutano huo itakosa kuibuka na mwafaka basi ifikapo tarehe 12 mwezi Septemba mwaka huu kaunti zote 47 nchini zitafungwa.
Katika kikao na Wanahabari, Oparanya ambaye pia ni Gavana wa Kakamega amesema serikali za kaunti zimekosa kutekeleza miradi ya maendeleo kufuatia kukwama kwa fedha hizo hali ambayo imechangia ugumu wa maisha kwa wananchi.
Bunge la Seneti limekosa kuafikiana kuhusu mfumo huo wa ugavi wa raslimali kwa serikali za kaunti katika vikao 9 vya bunge hilo na kupelekea kubuniwa kwa kamati maalum ya maseneta 12 kusawazisha mvutano huo na hadi sasa hakuna mwafaka ulioafikiwa.