Picha kwa hisani –
Huduma za kimatibabu katika hospitali na zahanati za umma Kaunti ya Mombasa, zimetatizwa pakubwa mapema leo, baada ya wauguzi katika Kaunti hiyo kugoma.
Katibu wa muungano wa wauguzi Kaunti ya Mombasa Peter Maroko, amesema japo Serikali ya Kaunti hiyo iliwalipa mishahara yao, bado kuna marupuru na maswala mengine msingi.
Maroko amesema malipo hayo hayawasaidii wauguzi na serikali ya Kaunti hiyo imeshindwa kulipa fedha za NHIF, akisema ni lazima maafikiano kati ya wauguzi hao na Serikali ya Kaunti ya Mombasa yazingatiwe, kabla ya wao kurudi kazini.
Kulingana na Maroko, wauguzi hao wamekuwa wakifanyia kazi katika mazingira magumu mno hasa wakati huu wa janga la virusi vya Corona, wakiwa bila ya vifaa maalum vya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.