Story by Salim Mwakazi –
Bodi ya hazina ya kitaifa ya Covid-19 ikishirikiana na wakfu wa Equity Bank imeweka wazi kwamba imetenga shilingi bilioni 1.4 kukabiliana na janga la Corona nchini.
Mwenyekiti wa bodi hiyo Dkt James Mwangi amesema fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa vifaa vya kupambana na ugonjwa wa Corona hasa kwa wahudumu wa afya nchini ili kuhakikisha visa vya maambukizi ya Corona vinadhibitiwa.
Akizungumza wakati wa halfa ya kuukabidhi vifaa vya kudhibiti maambukizi ya Corona usimamizi wa hospitali ya rufaa ya Msambweni kaunti ya Kwale, Dkt Mwangi ambaye pia ni Afisa mkuu mtendaji wa Benki za Equity amesema mpango huo utaendelea kwa muda wa miaka 3.
Kwa upande wake Gavana wa Kwale Salim Mvurya amesema vifaa hivyo vitasaidia kuwalinda wahudumu wa afya dhidi ya ugonjwa wa Corona huku akiwahimiza wakaazi kuendelea kuzingatia masharti ya kujikinga.