Picha kwa hisani –
Wakaazi wa eneo la Gumarey kaunti ya Wajir wamejawa na hofu baada ya kichwa cha naibu chifu aliyetekwa nyara na wanamgambo wa Alshabaab siku ya ijumaa juma lililopita kupatikana kando ya barabara.
Maafisa wa polisi wamesema kichwa cha afisa huyo tawala kwa jina Omar Adan Buul kimeonekana na wafugaji waliokua wanalisha mifugo yao katika eneo hilo na kwamba kwa sasa wanaendelea kuusaka mwili wa afisa huyo.
Katika kipindi cha majuma mawili yaliopita wanamgambo wa kundi la kigaidi la Alshabaab wameonekana kutekeleza mashambulizi katika eneo ambapo walivamia na kuharibu kituo cha polisi kabla ya kutoweka.
Kwa sasa maafisa zaidi wa usalama wametumwa eneo hilo kupiga doria ili kuzuia mashambulizi yanayopangwa kutekelezwa na magaidi hao.