Serikali ya kaunti ya Kwale imeidhinisha shilingi milioni 60 fedha zitakazogharamia mradi wa ujenzi wa kituo cha kutibu ugonjwa wa Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Msambweni.
Akihutubia Wananchi baada ya kufungua rasmi kituo cha kuhifadhi Damu yaani Blood Bank hospitalini humo, Gavana wa Kwale Salim Mvurya ameitaja hatua hiyo kama baadhi ya mikakati ya serikali ya kaunti ya Kwale kuboresha huduma za Afya.
Akijibu lalama za wananchi kuhusu huduma duni katika hospitali za umma katika kaunti ya Kwale, Gavana Mvurya amewaonya wahudumu wa afya wasiowajibika, akisema watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Kauli yake imeungwa mkono na Naibu Gavana Bi Fatuma Achani ambaye amehimiza uwajibikaji miongoni mwa maafisa wote wa umma wanaohudumu katika kaunti ya Kwale.
Mradi huo wa Kituo cha kuhifadhi damu uliogharimu shilingi milioni 32 umetekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya kaunti ya Kwale, Kampuni ya Base Titanium na Shirika la Maendeleo la Ujerumani GIZ.
Taarifa na Mariam Gao.