Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.
Mombasa, Kenya, Juni 8- Watetezi wa haki za kibinadamu mjini Mombasa wamekashfu vikali azma ya Wabunge ya kuikabili tume inayodhibiti mishahara na marupuru ya wafanyikazi wa umma nchini SRC kufuatia kauli yake ya kufika mahakamani kupinga marupurupu ya shilingi robo milioni ya nyumba kwa wabunge.
Watetezi hao wakiongozwa na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Haki Afrika Hussein Khalid wamesema kwamba Wabunge wa taifa hili wamekuwa walafi wa pesa na kushindwa kabisa kuwahudumia wananchi mashinani.
Katika mkao na wanahabari katika afisi za shirika hilo Mjini Mombasa, Khalid ameweka wazi kwamba watetezi hao wataunga mkono kivyovyote vile jitihada za tume hiyo za kupinga nyongeza hiyo akisema kwamba wananchi wanapitia mzigo mkubwa wa ushuru na nyongeza hiyo itazidi kuwakandamiza.
Aidha amepuuzilia mbali vitisho vya Wabunge hao akisema viongozi hao wamekosa maadili na hawawezi kuwatishia Wakenya wala vyombo vya habari kutokana na ulafi wao wa pesa.