Idara ya usalama imetakiwa kuidhinisha camera maalum za CCTV katika maeneo tofauti ya Gatuzi dogo la Kisauni ili kuwanasa wahalifu ambao wamewatia hofu Wakaazi wa eneo hilo.
Hii ni baada ya genge la vijana lifahamikalo kama ‘Wakali kwanza’ kuwajeruhi watu 11 huku wanne wakiwa katika hali mahututi katika hospitali kuu ya Ukanda wa Pwani katika uvamizi wa usiku wa kuamkia leo.
Afisa wa maswala ya dharura katika Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu Haki Afrika Hezron Shipetta amesema kupachikwa kwa camera hizo kutawasaidia Maafisa wa usalama katika kufuatilia kwa karibu kupitia mbinu za kiteknolojia shughuli mbalimbali katika eneo hilo lililozongwa na msururu wa visa vya uhalifu.
Kwa upande wake, Mwanaharakati wa kijamii kutoka Shirika la Mombasa ‘Women for Peace’ Bi Grace Oloo amesisitiza ni lazima wazazi wayawajibikie majukumu yao ipasavyo na kuwatahadharisha wazazi dhidi ya kuwaficha watoto wao wanaoshiriki uhalifu.
Akitoa kauli yake kuhusu matukio hayo, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la akina dada wanaopigania haki za kibinadamu la ‘Sisters for justice’ Bi Naillah Abdallah amesisitiza kukumbatia kwa polisi jamii katika eneo la Kisauni ili kuukabili uhalifu.