Picha kwa Hisani –
Huenda Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa akashtakiwa kwa makosa ya mauaji ya mwanamume mmoja wakati wa uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda kule Malindi kaunti ya Kilifi mwaka uliyopita.
Kulingana na Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Noordin Hajj, kesi ya mauaji ya Ngumbao Jolla ambaye alikuwa mjombake Reuben Katana aliyeshinda uchaguzi huo mdogo itaanza kusikizwa rasmi baada ya Jumwa kufanyiwa uchunguzi wa kiakili Jumatano juma lijalo.
Hajj, amesema ushahidi uliyowasilishwa katika afisi yake umetosha kumfikisha Jumwa ili kujibu mashtaka hayo ambapo Jolla alipigwa risasi na kufariki papo hapo baada ya purukushani lililozuka siku moja tu kabla ya uchaguzi huo mdogo.
Hata hivyo Inadaiwa kuwa Jumwa aliwasili katika makaazi ya Katana akitaka kufahamu kwa nini wanachama wa ODM bado walikuwa wakiendeleza kampeni za kisiasa licha ya kukamilika kwa muda wa kufanya kampeni hizo.
Jumwa alikanusha madai ya kuhusika na mauaji ya Jolla, akisema anahusishwa katika madai hayo ili kuzima ndoto yake ya kisiasa katika ulingo wa siasa nchini.