Familia moja katika eneo la Miritini Kaunti ya Mombasa imenusurika baada ya nyumba yao kuangukiwa na mbuyu kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika Kaunti ya Mombasa.
Mwenyekiti wa kitengo cha kukabiliana na majanga katika eneo hilo Bakari Ali Nyundo amesema kwamba mti huo umeng’oka na kuiangukia nyumba hiyo na kuiharibu kabisa usiku wa kuamkia leo.
Akizungumza katika eneo hilo, Nyundo amesema kwamba hali ingali tata hasa kutokana na taarifa kwamba viwango vya mvua vitazidi kuongezeka kwa siku tatu mtawalia kuambatana na utabiri wa idara ya utabiri wa hali ya anga nchini.
Shughuli za uchukuzi vile vile zimeathirika pakubwa katika Kaunti ya Mombasa baada ya barabara nyingi kufurika maji na madereva wa magari mengi ya uchukuzi wa umma kushindwa kumudu mafuriko hayo na kulazimika kuegesha magari yao.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.