Familia moja kutoka Nakuru inapigania haki baada ya binti yao kuuwawa katika hali tata katika eneo la Mishomoroni, Gatuzi dogo la Kisauni siku sita zilizopita.
Mamake marehemu Beatrice Wambui, Bi Rosemary Njeri amesema licha ya kufanya kila jitihada na kutafuta msaada kutoka kwa maafisa wa polisi, maafisa hao wamempuuza bila ya kumsaidia.
Njeri amehoji kwamba mwanawe alikuwa katika mgogoro wa kindoa na mumewe waliye zaa naye watoto wawili japo hadi sasa kilichopelekea mauaji hayo kingali kitendawili.
Kwa upande wake, Afisa wa maswala ya dharura katika Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini MUHURI Francis Auma amehoji kwamba visa vya mizozo ya kinyumbani Kaunti ya Mombasa vimeongezeka mara dufu.
Auma hata hivyo anawataka Maafisa wa usalama kuidhinisha uchunguzi wa dharura na kumtia nguvuni aliyehusika na mauaji hayo ili kuhakikisha kwamba familia ya Wambui inapata haki.