Story by Gabriel Mwaganjoni
Mshirikishi mkuu wa utawala kanda ya Pwani John Elungata amezindua shughuli ya kusaini kitabu cha rambirambi cha Rais watatu wa Kenya hayati Mwai Kibaki katika jumba la Uhuru na kazi kaunti ya Mombasa.
Wafanyabishara, Wakaazi na watu wa tabaka mbalimbali wamejitokeza ili kutia saini kitabu maalum cha kumuomboleza Kibaki nje ya jumba hilo.
Elungata amemtaja Kibaki kama Kiongozi muadilifu na aliyewajibikia maisha ya Wakenya katika uongozi wake wa kipindi cha muongo mmoja kama rais wa Kenya.
Wakati uo huo, baadhi ya Wakaazi na wafanyabiashara waliohudhuria zoezi hilo wametoa rambirambi zao kwa mwendazake Kibaki.
Huku hayo yakijiri ni siku ya mwisho kwa umma kuutazama mwili wa Kibaki katika Majengo ya bunge ambapo siku ya Ijumaa ibada ya wafu itaandaliwa katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi na kisha baadaye mwili huo kusafirishwa hadi nyumbani kwake Othaya kaunti ya Nyeri.
Kibaki atazikwa siku ya Jumamosi ambapo tayari Serikali imetangaza siku ya Ijumaa kuwa siku ya mapumziko kote nchini ili kutoa fursa kwa Wakenya kumuomboleza Kibaki.