Ni sharti bunduki iliyoibwa kutoka kwa Afisa wa polisi Hesbon Okemwa Anunda aliyeuwawa huko Lamu Mwezi Oktoba ipatikane.
Mshirikishi mkuu wa utawala katika Ukanda wa Pwani John Elungata amesema kwamba bastola hiyo iliyokuwa na jumla ya risasi 60 imo mikononi mwa watu hatari na huenda ikatumiwa katika kudidimiza usalama wa Kaunti hiyo.
Akizungumza Mjini Lamu, Elungata amesema oparesheni hiyo ya kusaka bastola hiyo aina ya G-3 kamwe haitasitishwa bali itaendelea hadi pale bastola hiyo na jumla ya risasi zake 60 vitakapopatikana kwani imewaweka Wakaazi wa Kaunti hiyo katika hatari.
Elungata amesema Idara ya usalama itawekeza oparesheni za kiusalama zitakazoangazia Kaunti za Tana River na Lamu ili kuhakikisha Kaunti hizo zilizo maeneo ya mipakani zinasalia salama.
Kifo cha Afisa huyo wa polisi huko Lamu yalipelekea oparesheni kali ya kiusalama na Wakaazi wa Lamu kupokea kipigo kutoka kwa Maafisa wa idara ya ulinzi KDF hali iliyopelekea watetezi wa haki za kibinadamu kuzuru Kaunti hiyo ili kulalamikia dhuluma hizo.