Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mshirikishi mkuu wa utawala kanda ya Pwani John Elungata amewaonya wakuu wa idara mbalimbali katika ukanda wa Pwani kwa kukosa kuhudhuria mikutano ya maendeleo pasi na sababu zozote msingi.
Elungata amesema baadhi ya wakuu wa idara hizo wamekuwa wakipuuzilia mbali mikutano ya kujadili kuhusu mchakato wa maendeleo katika ukanda wa Pwani chini ya kamati maalum ya utekelezaji wa maendeleo ya Serikali ya kitaifa inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, Elungata amesema ni kinyume kwa maafisa hao kuipuuza mikutano hiyo ambayo inatoa mwelekeo wa maendeleo mashinani, akihoji kwamba wale wanaokosa kuhudhuria mikutano hiyo wataadhibiwa.
Afisa huyo tawala amesema ni lazima maafisa hao wahudhurie mikutano hiyo ili wafahamu kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo na jinsi ya kushinikiza miradi hiyo ikamilishwe katika muda uliyowekwa.