Mashirika ya utetezi wa haki za kibinadamu Kaunti ya Mombasa yametakiwa kuliangazia mno swala la dhuluma za kijinsia na zile za kingono zilizokithiri mno katika eneo la Bangladesh huko Jomvu.
Wakaazi wa eneo hilo wakiongozwa na Mwanaharakati wa maswala ya kijinsia Bi Grace Bulaga wamesema eneo hilo kufuatia ukosefu wa huduma msingi limeshuhudia ongezeko la dhuluma hizo bila ya waathiriwa kufahamu hatua za kupigania haki.
Akizungumza huko Bangladesh wakati wa maadhimisho ya siku ya haki za kibinadamu ulimwenguni, Bi Bulaga amehoji kuwa licha ya jamii ya eneo hilo kudhulumiwa, haitambui jinsi inavyoweza kuzipigania haki hizo wala kupata msaada wowote kutoka kwa wanaofahamu sheria kikamilifu.
Kwa upande wake, Kiongozi wa kijamii wa eneo hilo Bi Pauline Auma amekiri kwamba swala la dhuluma za kijinsia na watoto wadogo kubakwa limekithiri mno katika eneo hilo.
Maadhimisho hayo ya siku ya haki za kibinadamu ulimwenguni yanatia kikomo siku 16 za uanaharakati zilizioanza Novemba 25 na zilizojumuisha maadhimisho mbalimbali yakiwemo siku ya walemavu, ile ya kupambana na ufisadi, kukabiliana na maambukizi ya virusi miongoni mwa kumbukumbu nyinginezo za kimataifa.