Story by Gabriel Mwaganjoni –
Dereva mmoja wa trela amefariki papo hapo huku kondakta wake akinusurika kifo baada ya kasha walilokuwa wakisafirisha kung’oka na kuangukia kichwa cha trela hilo.
Kulingana na Riaz Ahmed aliyeshuhudiwa mkasa huo wa mwendo wa saa kumi na moja katika eneo la Kiviwanda la Shimanzi Kisiwani Mombasa derava huyo amekuwa akijaribu kutafuta eneo la kuegesha trela hilo ili kushukisha mzigo wa nguo kuu kuu maarufu mitumba.
Kulingana na Riaz, kondakta wa trela hilo ameponea kwani alikua nje ya gari hilo akimsaidia dereva wake kuliegesha kabla ya kasha hilo kung’oka juu ya gari na kuangukia kichwa cha trela hilo na kusababisha maafa hayo.
Polisi ambao wameshuhudia ajali hiyo wameuchukua mwili wa Boniface Musyoka, dereva wa trela hilo mwenye umri wa miaka 32 na kuupeleka katika hifadhi ya maiti ya hospitali kuu ya rufaa kanda ya Pwani.