Muungano wa wanahabari wa michezo nchini umemtaja aliyekuwa mchezaji wa Zoo Kericho Denis Chetambe kama mchezaji bora wa mwezi Mei na Juni.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alipata jumla ya alama 17 huku akimpiku mpizani wake Boniface Muchiri wa klabu ya Tusker ambaye alipata alama 15 kwa mujibu wa muungano huo wa wanahabari.
Kiungo huyo mbunifu amekabidhiwa kikombe pamoja television ya inchi 42 kwa kuonyesha ueledi wake kwa kuisaidia timu yake ya Zoo kuepuka shoka la kushushwa daraja msimu uliopita kabla ya kujiunga na timu ya Bandari.
Kulingana na Muungano huo bado timu hiyo ya Bandari haija andikisha kandarasi mpya na mdhamini mkuu Sportpesa huku mchezaji huyo akitazamiwa kupokea shilingi laki 1 pindi timu hiyo itakapo andikisha kandarasi hiyo mpya.
Hata hivyo Chetambe hakuficha furaha yake baada ya kupokea tuzo hizo huku akisema kwamba zinampa changamoto kubwa za kuweza kufanya bidii na kunawiri Zaidi.
Kwa sasa Chetambe amesema kwamba kujiunga kwake na timu ya Bandari ni changamoto mpya huku akiutazamia upinzani mkubwa kutoka kwa wachezaji wenzake utakao msaidia kujiimarisha zaidi kisoka.
Kwa upande wake Naibu mkufunzi wa timu ya Bandari Solomon Mwakola ameusifia ujio wa kiungo huyo kwenye kikosi hicho huku akisema kwamba atasaidia pakubwa katika timu hiyo wanapo anza maandalizi ya mechi zao za ligi kuu nchini.