Aliyekuwa Mbunge wa Garsen Danson Buya Mungatana pamoja na wenzake sita wamefikishwa katika mahakama ya Malindi wakikabiliwa na takriban mashtaka 40 ya ufisadi.
Mbele ya hakimu mkuu Daktari Julie Oseko mahakama imearifiwa kuwa Mungatana pamoja na wenzake wakiwa wakurugenzi wa kampuni ya Zohali limited wanadaiwa kuilaghai serikali ya kaunti ya Kilifi takriban shilingi milioni tano na laki tatu.
Mahakama imearifiwa kuwa kampuni hiyo ilitoa fedha hizo mnamo tarehe tatu mwezi wa Oktoba mwaka wa 2016, kutoka kwa akunti ya kaunti ya Kilifi.
Hata hivyo wakili wa Mungatana Ndegwa Njiru ameambia mahakama kuwa mteja wake bado anaomboleza kifo cha mkewe aliyefariki hivi majuzi hivyo apewe muda wa wiki mbili kabla ya kujibu mashtaka dhidi yake huku akiongeza kuwa kama wakili hajapewa stakabadhi za upande wa mashtaka dhidi ya kesi hiyo.
Hata hivyo hakimu Julie Oseko amesema kuwa atapeana mwelekeo wa kesi hiyo iwapo washukiwa hao watasomewa mashtaka au la hapo baadae.