Story by Mimuh Mohamed-
Muungano wa vyama vya wafanyikazi nchini COTU umeitaka serikali kuu kuunda jopo maalum la wapatanishi watakaosaidia kusuluhisha mgomo wa marubani wa Shirika la ndege la Kenya Airways ulioingia siku ya nne hii leo.
Naibu Katibu mkuu wa COTU Benson Okwaro amesema majadiliano yana nafasi kubwa ya kusuluhisha mgomo huo, akisema kwa sasa taifa liko katika mgogoro wa kiuchumu na Kenya Airways ni kati ya kampuni itakayosuluhisha tatizo hilo.
Okwaro ameilaumu Wizara ya Leba nchini kwa madai kwamba imeshindwa kufanya mazungumzo na Shirika la Kenya Airways na Chama cha marubani nchini KALPA, ili kubuni mfumo maalum wa marubani kurejea kazini.
Mgomo huo wa marubani ulianza rasmi siku ya Jumamosi juma lililopita, ambapo marubani wameilaumu Kenya Airways kwa unyanyasaji, uongozi mbaya, kutoazingatia muongozo wa uchukuzi wa angani na kuondoa hazina ya akiba ya wafanyikazi.
Marubani 20 hata hivyo wamerejea kazini kufikia siku ya Jumatatu, huku Shirika la Kenya Airways likifutilia mbali jumla ya safari za ndege 40 zilizoratibiwa kuanza siku ya Jumatatu.