Story by Mwahoka Mtsumi –
Tume huru ya uchaguzi na mpaka nchini IEBC imesema itakata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa na Mahakama kuu kuhusu mchakato wa BBI kwamba tume hiyo haina makamishna wa kutosha kutekeleza majukumu yake.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati amesema uamuzi uliotolewa na jopo la majaji watano siku ya Alhamis juma lililopita unatofautiana na uamuzi uliotolewa na Mahakama kuu mwaka 2018.
Akizungumza na Wanahabari, Chebukati amesema Jaji wa Mahakama kuu Wilfridah Okwany mwaka wa 2018 katika uamuzi wake kuhusu majukumu ya IEBC, alisema Tume hiyo inaweza kutekeleza majukumu yake hata ikiwa na idadi ya Makamishna watatu kwa kuangazia kifungu cha 250 cha Katiba.
Itakumbukwa kwamba siku ya Alhamisi tarehe 13, Jopo la majaji watano akiwemo Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Chacha Mwita na Teresia Matheka, waliharamisha mchakato wa BBI kwa madai kwamba ni kinyume cha katiba.