Story by Our Correspondents-
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imesema imejipanga vyema kuhakikisha maandalizi ya uchaguzi mkuu ya Agosti 9 yanafanyika jinsi ilivyopangwa ili kuwawezesha wakenya kushiriki uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, amesema tume hiyo inakubali ukosoaji wa kisheria kuhusiana na maandalizi ya uchaguzi ili kuhakikisha mahali penye changamoto panatatuliwa kabla ya tarehe ya uchaguzi.
Katika kikao na Wanahabari jijini Nairobi, Chebukati amesema tume hiyo haitakiuka jukumu la uangalizi wa vyombo vya habari nchini kwani malengo ya IEBC ni kuhakikisha uchaguzi mkuu unakuwa huru na haki.
Chebukati aidha amesisitiza haja ya kujitolea kwa tume hiyo kufanikisha uchaguzi huo, akiweka wazi kwamba maafisa wa IEBC wako tayari kuhakikisha wananchi kutimiza jukumu lao la kikatiba.
Wakati uo huo amewaonya wanasiasa dhidi ya kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi, akisema atakayeenda kinyuma na maagizo ya IEBC atachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa muongozo wa sheria za uchaguzi.