Story by Gabriel Mwaganjoni
Japo bado mazungumzo yanaendelea kati ya Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya na Chama cha Wiper kuhusu uwezekano wa Kinara wa chama cha Wiper Stephen Kalonzo Musyoka kurudi tena kwenye muungano huo, kwa sasa Kalonzo ni mgombea wa urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Agosti, 9.
Haya ni kulingana na Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Wiper Balozi Chirau Ali Mwakwere aliyesema msimamo uliyoko kwa sasa ni kwamba Kalonzo ni Mgombea wa urais na endapo kutakuwa na mabadiliko yoyote basi wakenya watafahamishwa.
Katika kikao na Wanahabari katika kaunti ya Mombasa, Balozi Mwakwere amekariri kwamba ni usimamizi wa chama cha Wiper pekee uliyo na mamlaka ya kutangaza msimamo wa chama, akisema usimamizi wa chama hicho unapokea maoni ya wanachama kuhusu msimamo wa Kalonzo.
Kwa upande wake, Katibu mkuu wa chama cha Wiper Shakillah Abdallah amemkosoa mgombea wa urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga kwa kumhadaa Kalonzo licha ya kumuahidi kwamba angekuwa mgombea mwenza wake.