Picha kwa hisani –
Chama Cha ODM kimezifunga afisi zake katika Kaunti ya Tana River baada ya Chama hicho kukumbwa na mzozo wa uongozi.
Kulingana na Katibu Mkuu wa Chama Cha ODM Edwin Sifuna, uongozi wa Chama hicho katika Kaunti ya Tana River umekumbwa na mzozo kwa muda sasa, na wamechukua hatua ya kuzifunga afisi hizo ili kuutanzua utata huo.
Kulingana na Sifuna, tawi la Chama hicho katika Kaunti hiyo limekiaibisha Chama hicho kufuatia migogoro ya muda mrefu, akisema afisi za Chama hicho zitafunguliwa pale pande mbili pinzani zitakaposhirikiana.
Hata hivyo Gavana wa Kaunti ya Tana River Meja mustaafu Dhadho Godhana, ameulaumu uongozi wa Chama hicho chini ya Sifuna, ambao umeonekana kumuunga mkono Allan Dida, anayeongoza kundi pinzani la wafuasi wa Chama hicho, katika Kaunti hiyo ya Tana River.
Dhadho ametaka uchaguzi wa Chama hicho kuandaliwa nyanjani, ili kuwachagua viongozi wapya watakaoendeleza agenda ya Chama hicho, katika Kaunti ya Tana River.