Story by Mimuh Mohamed
Chama cha Maendeleo Chap Chap kimejiondoa katika Muungano wa Azimio la umoja na kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu rais William Ruto.
Akizungumza na Wanahabari, Kinara wa chama hicho ambaye pia ni Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua amesema Muungano wa Azimio la Umoja umekiuka mkataba wa makubaliano waliotia saini wakati wa kuundwa kwa muungano huo.
Mutua vile vile amesema kufikia sasa hawajapewa nakala za mkataba huo waliotia saini takriban mwezi mmoja uliopita, akihoji kwamba huenda viongozi wa Muungano wa Azimio la umoja wananjama za kubadili baadhi ya vipengele vya mkataba huo.
Mutua hata hivyo amedokez kwamba chama cha Maendeleo Chap Chap kimebaguliwa katika mipango yote ya kampeni za muungano wa Azimio la Umoja sawa na kutopewa ufadhili wa kifedha na kutoelezwa nafasi watakazopewa viongozi wa chama hicho iwapo Raila Odinga aliye Kinara wa muungano huo atafanikiwa kuingia ikulu.