Chama cha Jubilee, Wiper na CCM vimesaini mkataba wa makubaliano ya kufanyakazi pamoja ili kufanikisha huduma mbalimbali za maendeleo kwa wakenya wote
Akizungumza na Wanahabari katika makao makuu ya chama cha Jubilee jijini Nairobi baada ya makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Wiper Balozi Chirau Ali Mwakwere, amesema wakati umefika sasa kwa viongozi kuungana na kufanya kazi pamoja.
Naye Naibu Mwenyekiti wa Chama hicho, Mutula Kilonzo Junior, amesema makubaliano hayo yatafanikisha mikakati mbalimbali ya maendeleo nchini, sawia na mchakato wa BBI unaolenga kuleta mabadiliko mengi kwa wakenya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mashinani CCM, Isaac Ruto amewahakikisha wakenya kuwa viongozi hao watafanya kazi pamoja na serikali ya Jubilee ili kukamilisha miradi ya maendeleo ambayo haijakamilika.
Hata hivyo Rais Uhuru Kenyatta amewakilishwa na Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee David Murathe na Katibu mkuu wa Chama hicho Raphael Tuju wakati wa kutiwa saini nakala za mkataba wa makubaliano hayo.