Taarifa na Gabriel Mwaganjoni
Wizara ya usalama wa ndani imesema kuwa hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kufika katika bustani ya mama ngina mjini Mombasa kuanzia tarehe mosi ya mwezi Oktoba mwaka huu hadi wakati wa sherehe za mashujaa.
Katibu katika wizara hio Karanja Kibicho amesema ni Maafisa wa usalama pekee watakaokuwa wakisawazisha hali katika bustani hio hadi siku ya sherehe za Mashujaa inayoadhimishwa tarehe 20 ya mwezi Oktoba kila mwaka.
Kibicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya sherehe za kitaifa amesema shughuli za kupiga msasa maswala yanayofungamana na usalama na kurembesha kwa bustani hio zinaendelea na bustani hio itatumika kwa sherehe za kitaifa za Mashujaa mwaka huu.
Akihutubia wanahabari katibu huyo amesema bustani hio itakuwa huru kwa Wakaazi kuzuru na kujivinjari sawa na wafanyibiashara baada ya sherehe za Mashujaa za mwaka huu zitakazoongzwa na Rais Uhuru Kenyatta.
Amedokeza kwamba shughuli zote zikiwemo zile za burudani zitaongozwa na Wakaazi wa Ukanda wa Pwani huku wasanii wa kizazi kipya na wale wa kitamaduni kutoka ukanda wa pwani wakipewa kipau mbele.