Story by Mwahoka Mtsumi –
Bunge la Seneti limeupitisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka wa 2020 wa BBI bila ya kuufanyia marekebisho.
Hatua hiyo imetokana na uamuzi uliotolewa hapo awali na Spika wa bunge hilo Ken Lusaka kwamba bunge hilo halina uwezo wa kuvifanyia marekebisho baadhi ya vipengele katika mswada huo bali kupiga kura ya ndio au la.
Hata hivyo baada ya uamuzi huo wa Spika Lusaka, maseneta 51 wamepiga kura ya ndio, maseneta 12 wakipiga kura ya la huku seneta mmoja akikosa kuhudhuria kikao hicho cha kuudhinishwa kwa mswada wa BBI.
Akizungumza baada ya kupitishwa kwa mswada huo bungenii, Seneta maalum Christine Zawadi amewapongeza maseneta kwa kupitisha mswada wa BBI, akisema utachangia maswala muhimu mashinani.
Naye Seneta wa kaunti ya Kilifi Stewert Madzayo, amedai kuridhishwa na hatua ya maseneta kupitisha mswada wa BBI, akisema sasa ni jukumu la viongozi kuruzu mashinani na kuwarai wananchi kupitisha BBI wakati wa kura ya maamuzi.
Kwa upande wake Seneta wa Siaya James Orengo amesema licha ya maseneta kupitisha mswada huo jukumu lililosalia sasa liko chini ya wananchi kuamua hatima ya BBI wakati kura ya maamuzi.
Sasa ripoti ya mswada huo itawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kuidhinisha kabla ya Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kuandaa tarehe maalum ya kura ya maamuzi.