Bunge la Seneti linafuatilia kwa karibu mno shughuli katika kivuko cha feri cha Likoni ili kuhakikishia usalama watumizi wa kivuko hicho.
Kulingana na Seneta wa Kaunti ya Mombasa, Mohammed Faki, kivuko hicho katika kipindi cha mwaka uliyopita kimekabiliwa na changamoto nyingi mno, huku watumizi wakiingiwa na hofu kufuatia ajali za mara kwa mara kivukoni humo.
Akizungumza mjini Mombasa, Faki amesema kwamba feri ya MV- Safari ambayo imekuwa ikijengwa nchini Uturuki itawasili katika kivuko hicho baadaye mwezi huu wa Februari au mwanzoni mwa mwezi Machi na inatarajiwa kusaidia pakubwa katika kuziboresha shughuli katika kivuko hicho.
Kiongozi huyo amehoji kwamba ni sharti shughuli katika kivuko hicho ziangaziwe hasa ikizingatiwa kwamba kivuko hicho huunganisha taifa hili na lile jirani la Tanzania.
Kauli ya Faki inajiri huku hali ya msongamano ikikikumba kivuko hicho hasa baada ya feri mbili za MV-Likoni na MV- Nyayo kuondolewa kivukoni humo ili kufanyiwa ukarabati.