Story ya Mimuh Mohamed –
Bunge la kitaifa limemuidhinisha Jaji Martha Koome kuchukua nafasi ya jaji mkuu nchini, baada ya kujadili ripoti iliowasilishwa katika bunge hilo na kamati ya bunge kuhusu haki na sheria JLAC baada ya kumpiga msasa wa Jaji Koome.
Kwenye kikao kilichoongozwa na naibu spika Moses Cheboi wabunge kwa kauli moja wameunga mkono ripoti hiyo ya kamati ya JLAC chini ya mwenyekiti wake Muturi Kigano iliyopendekeza kuidhinishwa kwa Jaji Koome.
Wakati wa kujadili ripoti hiyo wabunge akiwemo mbunge wa Rabai William Kamoti wamemshauri Jaji Koome kuangazia masuala ya jinsia ikiwemo haki za wanaume na kumaliza ufisadi katika idara ya mahakama.
Kwa upande wake mbunge wa Garissa mjini Adan Duale amemtaka Jaji Koome kufuata nyayo za Jaji mkuu mstaafu David Maraga naa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria.
Kwa sasa bunge litawasilisha jina la Jaji Koome kwa Rais Uhuru Kenyatta ili kuchaguliwa rasmi kuwa Jaji mkuu nchini.