Bunge la kaunti ya Tana River limemtimua Mamlakani Spika wa bunge hilo Michael Justine Nkaduda.
Katika hoja iliyowasilishwa bungeni humo na Mwakilishi wa Wadi ya Mikinduni Mohammed Buya, Wawakilishi Wadi wote 20 wameipitisha hoja hiyo bila kupingwa wakimkosoa Nkaduda kwa kulumbana na Gavana wa kaunti hiyo Meja Mstaafu Dhadho Godhana.
Buya amesema tangu mwaka wa 2017 alipoingia mamlakani, Nkaduda amedidimiza maendeleo ya kaunti hiyo kwa kukosa kushirikiana na bunge hilo wala Gavana wa kaunti hiyo katika kuangazia maswala ya maendeleo.
Kauli ya Buya imeungwa mkono na Kiongozi wa wachache katika bunge hilo Abdi Argamso anayeshikilia kwamba Spika Nkaduda amekuwa akiendeleza kampeni za mwaka wa 2022 na kuyaweka kando majukumu yake.
Kwa sasa, kamati ya wajumbe watano itateuliwa ili kumsikiliza Nkaduda kuhusu lawama za utepetevu na ubinafsi anazolimbikiziwa na wajumbe hao na kisha baadaye hoja hiyo kurudi tena bungeni na endapo itaidhinishwa na bunge hilo basi moja kwa moja Nkaduda itakuwa imetimuliwa.