Picha kwa hisani –
Bunge la kaunti ya Siaya, ni bunge la kwanza kuujadili na kuupitishwa mswada wa BBI ili kufanikisha mchakato wa kuifanyia marekebisho Katiba.
Spika wa bunge la kaunti ya Siaya, George Okode, amesema bunge hilo limeujadili na kuupitisha mswada huo bila ya pingamizi na sasa watawasilisha stakabadhi za kuidhinishwa kwa mswada huo mbele ya bunge la kitaifa.
Akizungumza na Wanahabari baada ya bunge la kaunti hiyo kuupitisha mswada huo, Gavana wa Siaya Cornel Rasanga amewapongeza Wawakilishi wadi wa kaunti hiyo, akisema hatua walioichukua itafanikisha manufaa mengi kwa wananchi wa kaunti ya Siaya.
Hatua ya bunge hilo limejiri siku moja tu baada ya Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, kusalisha nakala za mswada huo katika mabunge yote 47 ya kaunti.
Kwa mujibu wa Tume ya IEBC, iwapo mswada huo utapitishwa na mabunge ya kaunti 24 basi moja kwa moja utawasilishwa katika bunge la kitaifa na seneti ili kuidhinishwa na kuandaliwe kura ya maoni nchini.