Mwakilishi wa Wadi ya Mikindani kaunti ya Mombasa Juma Renson Thoya, sasa anataka uchunguzi kufanywa kuhusiana na vifo vya watu wawili vinavyodaiwa kuchangiwa na bohari la kuhifadhi bidhaa ya Klinker inayotumika kutengeneza Simiti katika eneo hilo.
Thoya amesema ni lazima uchunguzi wa kina kufanywa na familia za watu hao kufidiwa.
Akizungumza kule Mikindani, Thoya ameitaka Serikali kuu kuchunguza hati miliki ya ardhi ya kampuni ya ‘Motrex’ inayomiliki bohari hilo, akisema hati miliki hiyo huenda ilipatikana kwa njia za wizi.
Aidha amekariri kuwa vumbi kali linalotokana na shughuli katika bohari hilo limepelekea madhara makubwa ya kiafya kwa Wakaazi pamoja na kusambaratisha shughuli za Kilimo katika eneo hilo. Tayari Serikali ya kaunti ya Mombasa imeapa kuifunga kampuni hiyo iwapo haitazingatia swala la Afya na Mazingira ya wakaazi wa eneo hilo.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.