Baraza la Magavana nchini limeziagiza serikali zote za kaunti, kuwatuma wafanyikazi wake kwa likizo ya wiki mbili sawia na kusitisha utoaji wa huduma ambazo sio muhimu kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Baraza hilo Wycliffee Oparanya amesema utata unaozingira ugavi wa raslimali kwa serikali za kaunti umechangia hali ngumu ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Oparanya amedokeza kuwa kutokana na kaunti hizo kukosa pesa za kuendesha shuhuli zake, hakuna wagonjwa zaidi ambao watalazwa hospitalini na wagonjwa ambao watafika hospitalini kutibiwa na kuondoka watakuwa wachache mno.
Hii inafaa kuafikiwa kabla ya Septemba 18 siku ya Alhamis mwaka huu, ambapo serikali za kaunti zimepanga kusitisha huduma zote kutokana na kukosa fedha za kuwajibikia huduma za kaunti.
Haya yamejiri baada ya maseneta siku ya Jumanne katika kikao cha bunge la Seneti kukosa kuafikiana kwa mara ya 10 kuhusu mbinu inayofaa kutumika katika kugawanya raslimali kwa serikali za kaunti.