Story by Gabriel Mwaganjoni –
Baraza la mashauri ya Kiislamu nchini KEMNAC limeidhinisha mpangilio maalum wa Afisi ya Kiongozi mkuu wa jamii ya Waislamu anayejulikana kama Mufti ili kuondoa mgawanyiko ambao umeikumba jamii hiyo kwa muda sasa.
Katika kikao na Wanahabari mjini Mombasa Mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Juma Ngao amesema mpangilio huo wa Mufti mkuu nchini sawa na mufti wengine 47 katika kaunti zote nchini utasawazisha maswala tata katika dini hiyo ikiwemo muandamo wa mwezi wa Ramadhan.
Sheikh Ngao amesema malengo makuu ni kuwaleta waislamu pamoja, kujadili mwelekeo wa dini hiyo na kutanzua maswala ambayo huenda yakazua utata miongoni mwa wafuasi wa dini hiyo.
Wakati uo huo, Mwenyekiti huyo wa KEMNAC amesema Mufti hao watafunzwa rasmi kuhusu majukumu yao ili wayatekeleze vyema mashinani.