Shughuli za uchimbaji na usafirishaji mchanga kule Mjanaheri kaunti ndogo ya Magarini zinaendelea kusambaratika kila kukicha kutokana na barabara mbaya ambayo imepelekea magari ya kubeba mchanga kukwama na mengine kusitisha shughuli za kusafirisha bidhaa hiyo.
Faki Munga pamoja na Safari Karema ambao ni wa wadau wa sekta hiyo ya mchanga wamesema kuwa barabara hiyo ya Ngomeni na ambayo inaunganisha timbo hizo za mchanga ni mbaya mno na kwamba inafaa kukarabatiwa mara moja.
Wanadai kuwa mamia ya lori za mchanga hukwama kila uchao licha ya kuwa wanatozwa ushuru kwa kila lori litalobeba mchanga katika eneo hilo wakidai kuwa hali yao ya Maisha sasa imeanza kusambaratika.
Kwa sasa wanaitaka serikali ya kaunti ya Kilifi ishirikiane mara moja na serikali kuu ili barabara hiyo iweze kukarabatiwa na shughuli za kawaida ziweze kuendelea.