Klabu ya Bandari imedidimiza matumaini ya klabu ya Gor Mahia ya kumaliza msimu bila kushindwa kwa kuilaza mabao 2-1.
Bandari wameivunja rekodi hiyo kwa kuandikisha ushindi kwenye mechi kali iliyochezwa katika uga wa Mbaraki Sports Club mjini Mombasa, Jumanne.
Bandari walianza mashambulizi katika dakika ya 12 kupitia Dan Guya aliyemdakisha nzi kipa wa Gor na kuwaeka Bandari kifua mbele.
Mashambulizi ya Bandari yaliendelezwa na Yema Mwana na kuzaa matunda katika dakika ya 36.
Katika kipindi cha pili timu zote mbili zilijikaza kibwebwe licha ya wachezaji kushuhudia joto kali na ugumu mkubwa wa mechi. Kutokana na patashika hiyo Fred Nkata alipatiwa kadi ya njano ya pili iliyopelekea kwake kupata kadi nyekundu na kutolewa uwanjani. Dan Guya alikimbizwa hospitalini baada ya kupata jeraha alipochezewa visivyo na Haron Shakava.
Klabu ya Gor Mahia imepata la kufutia machozi kupitia kwa Jacquis Tuyisenge.
Timu hizi zimekutana mara 18 Gor Mahia wakishinda mara tisa, na kuandikisha sare mara nne.
Kwa sasa klabu ya Bandari inakwea jedwali la msimamo wa ligi hadi nambari 2 wakiwa na pointi 45, pointi 11 nyuma ya Gor Mahia na pointi mbili mbele ya Sofapaka.
Taarifa na Dominick Mwambui.