Story by Gabriel Mwaganjoni –
Bandari ya Lamu inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi juma hili baada ya vifaa vya kunyanyua shehena kutoka melini sawia na kuzipakia kwenye matrela kuwasili katika bandari hiyo.
Mshirikishi mkuu wa Ukanda wa Pwani John Elungata, amesema mitambo hiyo maalum iliwasili Lamu juma lililopita, huku mingine ikiwasili Jumatatu hii baada ya kupakiwa melini katika bandari ya Mombasa.
Elungata amesema vitengo vitatu kati ya 32 vya bandari hiyo vimekamilika na meli kubwa zinatarajiwa kuanza kuegeshwa katika bandari hiyo hali itakayopanua uchumi wa nchi na mataifa jirani ikiwemo Ethiopia.
Akizungumza alipozuru bandari hiyo ya Lamu, Elungata amesema miundo msingi ya kusafirisha shehena kutoka bandarini humo pia imekamilika huku ujenzi wa barabara ya kutoka Lamu, Garsen, Garissa hadi Isiolo ukielekea kukamilika.
Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzindua shughuli za bandari ya Lamu siku ya Alhamis juma hili.