Story by Mimuh Mohamed–
Mgombea wa kiti cha ugavana wa kaunti ya Kwale kupitia chama cha WIPER Balozi Chirau Ali Mwakwere amesema hivi karibu atamtangaza kwa umma mgombea mwenza wake ili wakaazi wa kaunti hiyo wawe na ufahamu wa kina.
Balozi Mwakwere amesema amechagua mgombea mwenza muadilifu na mwenye tajriba ya kutosha atakayewajibikia majukumu yake kikamilifu na kufanikisha maendeleo ya kaunti ya Kwale.
Akizungumza wakati wa mahojiano ya kipekee na kituo cha Radio Kaya, Balozi Mwakwere amesema hatua aliyochukuwa ya kuchagua mgombea mwenza kutoka jamii ya wakamba inalenga kuhakikisha jamii zote za kaunti ya Kwale zimejumuishwa katika uongozi wa kaunti hiyo.
Balozi Mwakwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha WIPER amesema tayari chama hicho kimewapa baadhi ya wagombea tiketi za chama hicho kuwania nafasi ya useneta na uwakilishi wa kike katika kaunti ya Kwale wakati wa uchaguzi mkuu.
Akigusia tetesi zinazoenezwa kuhusu aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko kuwania ugavana wa Mombasa kupitia chama cha WIPER, Balozi Mwakwere amesema watatoa tamko rasmi kufikia siku ya Jumamosi juma hili.