Story by Our Correspondents
Chama cha WIPER kimewakabidhi rasmi tiketi ya chama hicho baadhi ya wagombea wa viti vya ugavana nchini ili kujitosa katika kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Kati ya wale waliopewa tiketi ya chama hicho ni pamoja na mgombea wa kiti cha ugavana wa kaunti ya Kwale Balozi Chirau Ali Mwakwere, Mutula Kilonzo Junior anayegombea kiti cha ugavana wa Makueni na Mike Mbuvu Sonko anayegombea kiti hicho kaunti ya Mombasa.
Viongozi hao wamekabidhiwa tiketi ya chama hicho na Kinara wa Chama cha WIPER Kalonzo Musyoka aliyesema hatua hiyo itafanikisha uongozi bora nchini kwani viongozi waliopewa tiketi hiyo wana tajriba ya kisiasa.
Hata hivyo Kalonzo ametoa tiketi ya chama hicho kwa Prof. Philip Kaluki kuwa mgombea mwenza wa Polycarp Igathe anayelenga kuwania kiti cha ugavana wa Nairobi wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Wakati uo huo viongozi wa chama hicho wameishinikiza kamati ya Muungano wa Azimio la umoja One Kenya iliyobuniwa kuteua mgombea mwenza wa Odinga kuzingatia tajriba ya Kalonzo wakisema iwapo Odinga na Kalonzo watashikilia serikali basi taifa hili litapiga hatua kimaendeleo.