Story by Our Correspondents –
Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Wiper Balozi Charau Ali Mwakwere, amesema mizozo ya ardhi, ukosefu wa maji safi na uchumi duni kwa wakaazi wa eneo bunge la Kinango umechangiwa na viongozi wasiowajibika.
Mwakwere aliyetangaza nia yake ya kuwania kiti cha ugavana wa kaunti ya Kwale wakati wa uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka huu, amewahakikishia wakaazi wa Kinango kwamba changamoto hizo zitatatuliwa iwapo atachaguliwa.
Mwakwere aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa kuchagua kamati za kuendesha kampeni za chama cha Wiper katika maeneo ya Puma, Ndavaya na Macknon Road ameahidi kuwahudumia wakaazi wa kaunti ya Kwale bila kujali ukabila, dini wala siasa za maeneo.
Wakati uo huo amewataka wakaazi wa kaunti ya Kwale kutokubali kuhadaiwa kifedha na kuwachugua viongozi wasio na malengo ya maendeleo, akisema viongozi kama hao ndio wanaorudisha nyuma maendeleo mashinani.
Kwa upande wake Mgombea wa kiti cha uwakilishi wa wadi ya Puma katika kaunti hiyo Mrinzi Nyundo, amempigia debe Mwakwere kunyakuwa kiti cha ugavana wa Kwale wakati wa uchaguzi mkuu, akisema kaunti ya Kwale inahitaji viongozi wasio na rekodi ya ufisadi.