Story by Ali Chete-
Mbunge wa Jomvu Badi Twalib amemtaka Waziri wa Elimu nchini Prof. George Magoha kuweka mikakati endelevu katika swala la elimu nchini na kufanya masomo ya shule za upili kuwa bila malipo.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa wakati wa kutoa fedha za basari kwa wanafunzi wa shule za upili katika eneo bunge lake, Badi amemtaka Waziri Magoha kuangazia maslahi ya wanafunzi wanaotoka katika familia zisizojiweza ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa kuhudhuria masomo.
Badi amesema serikali inafaa kuweka mikakati bora itakayochangia shule za upili kuwa za bila malipo jinsi serikali inavyoshinikiza swala la asilimia 100 ya wanafunzi kujinga na kidato cha kwanza.
Wakati uo huo ameitaka serikali ya kitaifa kupitia bodi ya nafaka nchini kusambaza chakula kwa shule zote za umma hali ambayo itapunguza mzigo wa karo kwa mzazi.