Picha kwa hisani
Staa wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz ametoa kauli kwa mara ya kwanza baada ya mama yake mzazi, Bi Sandrah kusema kuwa mzee Abdul si baba mzazi wa Diamond. Habari kubwa wiki iliyopita kwa mashabiki wanaofuatilia maisha yasiyoisha visa na mikasa ya msanii wa muziki wa Bongo flava kutoka Tanzania, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ ilikuwa ni taarifa kwamba mtu anayefahamika kuwa ni baba mzazi wa Diamond, mzee Abdul Isaack sio baba yake mzazi.
Mama Dangote alipasua kwamba baba mzazi wa Diamond si mzee Abdul kama ilivyokuwa inafahamika na wengi na badala yake alisema baba wa damu wa msanii huyo anaitwa Salum Nyange ambaye kwa sasa ni marehemu.
Hata hivyo, Diamond amekuwa kimya kwa kipindi chote cha sekeseke hilo lakini leo amelizungumzia kwa mara ya kwanza.
Akijibu moja ya maswali katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika juzi, Januari 19 kwenye ofisi za Wasafi TV na Redio kwa ajili ya kuongelea tamasha la Tumewasha, Diamond amesema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa badala yake atatafuta muda wa kujibu.
“Samahani sana mwandishi, siwezi kuongelea mambo ya kitandani hapa. Naomba kaa na swali lako, nitakuja kujibu yote siku sio nyingi,” amesema Diamond.
Vuta n’kuvute ya nani baba wa damu wa msanii huyo imeendelea kuwa na joto kali haswa kwenye mitandao ya kijamii.