Story by Mwahoka Mtsumi –
Baadhi ya Wanasheria kutoka ukanda wa Pwani sasa wanapendekeza kufanyiwa marekebisho kwa sheria za ardhi nchini ili kumuwezesha mkaazi wa Pwani kumiliki ardhi pasipo na usumbufu wowote.
Wanasheria hao wakiongozwa na Wakili George Kithi wamesema bado serikali inatumia sheria za tangu enzi za ukoloni ndiposa mizozo ya ardhi imekosa suluhu la kudumu na kuendelea kushuhudiwa kwa migororo ya ardhi.
Wakili Kithi amesema iwapo sheria za ardhi nchini zitafanyiwa marekebisho na kuzingatiwa kwa mipaka inayotambuliwa na wazee basi mizozo ya ardhi katika ukanda wa Pwani itapata suluhu na wakaazi kupata hati miliki.
Wakati uo huo amesisitiza haja ya kutumika kwa historia za umiliki wa ardhi katika kutatua mizozo ya ardhi kanda ya Pwani huku akipendekeza eneo la Pwani kuwa na sheria maalum ya umiliki wa ardhi.