Picha kwa Hisani –
Katibu mkuu msimamizi katika Wizara ya Afya nchini Dkt Rashid Aman amewaonya vijana dhidi ya tabia ya kupuuza masharti ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona kwa kisingizio kuwa hawawezipata virusi hivyo.
Dkt Aman amesema asilimia 70 ya idadi ya wakenya ni vijana na wako katika hatari ya kupatwa na virusi hivyo iwapo hawatakuwa waangalifu na kuzingatia masharti ya kiafya.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa Shirika la IGAD Dkt Workneh Gebeyehu, amesema shirika hilo inakabiliana kikamilifu na changamoto za usalama wa chakula hasa kwa wakimbizi ili kudhibiti maambukizi.
Hata hivyo Wizara ya Afya nchini imedokeza kuwa watu 271 wamethibitishwa kupata virusi vya Corona baada ya sampuli 4,019 kufanyiwa uchunguzi na kupelekea idadi hiyo kuongezeka hadi watu 30,636.
Wizara hiyo imesema kati watu hao 271, watu wanne ni raia wa kigeni na 267 wakiwa wakenya huku mtoto wa mwaka mmoja ni kati ya wale walioambukizwa virusi hivyo.
Wakati uo huo Wizara hiyo imesema watu 208, wamepona virusi hivyo na kupelekea idadi ya waliopana nchini kufikia watu 17,368 huku watu watano wakiaga dunia kutokana na virusi hivyo.