Story by Ephie Harusi –
Shirika la Perfomance Monitoring for Action limesema utafiti uliofanywa katika kaunti ya Kilifi kuhusu Afya umeonyesha wazi kwamba asilimia 49 ya Wanawake katika kaunti hiyo wamekumbatia mpango wa kupanga uzazi.
Kulingana na Mkuu wa utafiti wa Shirika hilo Prof Peter Gichangi, idadi hiyo imeongezeka kutoka asilimia 34 mwaka 2014 baada ya utafiti kufanywa kwa akina mama wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi miaka 49.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo mjini Kilifi, Prof Gichangi amesema asilimia 8 ya wasichana wadogo wanaovunja ungo wamekumbatia mpango huo baada ya kubainika wazi kwamba asilimia kubwa ya wasichana hao wameanza kujihusisha kimapenzi.
Prof Gichangi amesema ipo haja ya akina mama na wanandoa kuelezwa kuhusu mbinu mpya za kupanga uzazi baada ya kubainika kuwa asilimia 60 ya akina mama hawajawahi pata mafunzo hayo.
Kwa upande wake mshirikishi wa afya ya uzazi kaunti ya Kilifi Kenneth Miriti amesema amewashauri wanaume kuhusishwa katika mpango wa afya ya uzazi.