
Arnold Origi akipeana vifaa vya michezo kwa watoto Kwale.
Aliyekuwa kipa wa timu ya taifa soka nchini Harambee stars Arnold Origi, ameihimiza jamii ya kaunti ya Kwale kukuza talanta ya michezo miongoni mwa watoto ili kuwaepusha na visa vya uhalifu na utumizi wa mihadarati.
Akiongea katika uwanja wa michezo ya Kombani alipokutana na watoto wenye umri chini ya miaka 12 wanaochezea timu mbalimbali kupitia udhamini wa shirika la Samba Sports, Origi amewapa wazazi changamoto kutambua vipaji vya watoto wao na kuvikuza.
Amesema kuwa maeneo ya miji ikiwemo Nairobi ikiendelea kuwapa watoto motisha wa kuboresha vipaji vyao katika michezo, maeno ya mashimani yangali yamesalia nyuma, huku akiongeza kuwa ameanza kuzuru sehemu hizo za mashinani, kuhamasiha jamii kuhusu umuhimu wa michezo.
Mchezaji huyo aidha amedokeza kuwa mbali na kufungua mlango wa maendeleo maishani, michezo inaweza kutumika kama kampeni ya kuwahamasisha vijana kuhusu athari za makundi ya kihalifu, utumizi wa mihadarati , mimba na ndoa za mapema miongoni mwa wasichana wadogo.
Taarifa na Michael Otieno.