Ali Khamis maarufu kama Ally-B amewasihi Vijana wa Kaunti ya Mombasa kujitenga na magenge ya kihalifu.
Msanii huyo maarufu ameitaja hali inayoyakumba maeneo ya Kisauni katika Kaunti hiyo kama ya kusikitisha mno ambapo sasa vijana wamekuwa wakiwauwa wakaazi na kuwalenga zaidi wanaharakati wa amani na maafisa wa polisi hali iliyosababisha hofu miongoni mwa wakaazi wa eneo hilo.
Akizunngumza katika eneo la Kisauni Kaunti ya Mombasa, Ally-B amesema kwamba japo huenda swala la mihadarati na ukosefu wa ajira limeachangia katika hali hiyo, kamwe haimakiniki kwa Vijana kuwavamia wakaazi na kuwakata kata kwa mapanga wakiwaibia na kuwauwa.
Msanii huyo anayefahamika vyema kwa vibao vyake kama vile ‘Maria’ na ambaye pia ni Mwanaharakati wa Vijana Pwani hata hivyo amewakosoa wazazi kwa kuyatelekeza majukumu yao akisema kwamba pengo kati ya watoto na wazazi ndicho kiini cha kupotoka kimaadili kwa kizazi kichanga katika Kaunti hiyo ya Mombasa.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.