Maafisa wa Shirika la uhifadhi wa wanyama pori nchini KWS wanamzuilia mtu mmoja aliyenaswa na vipepeo vilivyokaushwa na manyoya ya ndege aina ya kanga katika mpaka wa Kenya na Tanzania eneo la Lungalunga Kaunti ya Kwale.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari jioni ya leo kutoka kwa Mamalaka ya ushuru nchini KRA, Mwanamume huyo alikuwa akisafiri kutoka Tanga hadi Mjini Mombasa akiwa na jumla ya vipepeo hivyo 210 na vurushi 20 vya manyoya ya kanga.
Maafisa hao wamethibitisha kwamba shehena hiyo ilikuwa ikitoka Dar-es-Salaam ikielekezwa mataifa ya Hungary na Uingereza huku mmiliki huyo akikosa cheti chochote kutoka kwa Shirika hilo cha kumruhusu kutekeleza shughuli hizo.
Vile vile Mwanamume huyo aliyetiwa nguvuni asubuhi ya leo, alikuwa anamiliki muhuri kutoka kwa Mkurugenzi wa tiba ya mifugo Jijini Dar-es-Salaam, nchini Tanzania.
Maafisa hao wa KWS katika eneo hilo la Lungalunga wanaendelea kumhoji jamaa huyo huku wakiizuilia shehena hiyo ya manyoya ya kanga na vipepeo vilivyokaushwa kabla ya kumfikisha mahakamani.