Picha kwa hisani –
Dereva mmoja wa gari dogo la kibinafsi amenusurika kifo baada ya kuangukiwa na kasha lililong’oka juu ya trela katika eneo la Kibarani kwenye barabara kuu ya Mombasa – Nairobi.
Akithibitisha tukio hilo Afisa mkuu wa polisi eneo la Changamwe Joseph Kavoo amesema gari hilo dogo sawa na trela hilo zote zilikuwa zikielekea upande wa Changamwe ambapo kasha hilo lililokuwa na mafuta ya kupikia limeteleza kutoka juu ya trela na kuliangukia gari hilo dogo aina ya Premio.
Gari hilo dogo lilikuwa na dereva pekee aliyenusurika na kupata majeraha madogo, huku Wakaazi wakiyaiba mafuta yote ya kupikia yaliyokuwa kwenye kasha hilo.
Kavoo amewataka madereva kuwa makini hasa wanapokaribia eneo hilo la Kibarani ambalo linashuhudia shughuli nyingi za ujenzi wa barabara hiyo.
Ajali hiyo imechangia msongamano mkubwa wa magari kwani trela hilo limeifunga kabisa barabara hiyo na kuzuia magari ya pande zote mbili kupita.