Chama cha ODM kupitia kamati ya nidhamu ya chama hicho sasa kinataka Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Msabweni Suleiman Dori wafurushwe kwenye chama hicho.
Katibu wa chama hicho Edwin Sifuna amesema kuwa wawili hao pamoja na wawakilishi 6 wa wadi kutoka kaunti za Homa Bay na Busia wanafaa kufurushwa chamani kwa kutofuata masharti ya chama hicho sawa na kutomuheshimu kinara wao Raila Odinga.
Pendekezo hilo linajiri baada ya Aisha, Dori na wawakilishi hao kutangaza hadharani azma yao ya kumuunga mkono Naibu wa rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022.
Hatima ya wawili hao sasa inasalia mikononi mwa kamati kuu ya ODM ambayo itaidhinisha iwapo wafurushwe chamani au la.
Taarifa na Mimu Mohammed.