Afisa wa idara ya huduma za jamii eneo la lungalunga Enock Masita amefikishwa katika mahakama ya Kwale baada ya kukamatwa siku ya Jumatano kwa madai ya kumnajisi msichana mwenye umri wa miaka 17, mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya upili ya wasichana ya Mwangeka kaunti ya Taita Taveta.
Akithibitisha kisa hicho afisa mkuu wa polisi eneo la Matuga Joel Chesire amesema kuwa Masita anadaiwa kutekeleza unyama huo siku ya Jumamosi katika nyumba moja ya malazi ya wageni mjini Kwale.
Chesire amesema kwamba msichana aliyenajisiwa ni yatima katika nyumba ya Watoto ya upendo huko Matuga ambapo afisa huyo wa huduma za jamii huwatembelea na kuwapa misaada kutoka kwa serikali .
Chesire amekilaani kisa hicho akiwaonya maafisa wengine wa serikali wanaoendeleza dhulma kwa jamii kuwa wataadhibiwa vikali.
Kwa upande wake mtetezi wa haki za kibinadamu wa shirika la Haki Afrika tawi la Kwale Alexander Mbela ametaka mshtakiwa kuadhibiwa vikali ili haki ipatikane kwa mwathiriwa.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya mbunge wa Matuga Kassim Sawa Tandaza kutaka wanaume wanaotekeleza visa vya unajisi kuhasiwa.